Japani yaongeza maradufu idadi ya watu wanaowasili ikizidi kulegeza udhibiti wa virusi vya korona mipakani

Japani imeongeza zaidi ya maradufu ukomo wa idadi ya watu wanaowasili kila siku ikizidi kulegeza vikwazo vyake vya virusi vya korona vya kuingia nchini humo.

Kuanzia leo Jumatano, ukomo wa idadi ya wanaowasili nchini humo kila siku imeongezwa hadi kufikia 50,000 kutoka 20,000.

Wote wanaowasili ikiwa ni pamoja na raia wa Kijapani, watasamehewa kuonyesha uthibitisho wa kipimo cha kutokuwa na virusi vya korona ikiwa wamepata chanjo ya dozi ya tatu ya virusi hivyo.

Watalii wote wa kigeni wanaruhusiwa kusafiri nchini Japani bila ya kuwa na waongozaji. Hilo linachukua nafasi ya sheria inayosema ni watalii kutoka mataifa na maeneo yaliyochaguliwa tu ndio wanaruhusiwa kuingia Japani, na wanatakiwa kujiunga na safari zenye waongozaji.

Serikali ya Japani ilisema kwamba inalenga kuweka uwiano kati ya hatua za kuzuia maambukizi na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Waziri Mkuu Kishida Fumio mapema alielezea matumaini yake ya kulegeza zaidi hatua hizo hadi kuwa sawa na viwango vya mataifa mengine ya Kundi la nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani. Alisema angefanya maamuzi baada ya kufanya tathmini ya hali ya maambukizi ndani na nje ya nchi pamoja na matakwa na hatua za udhibiti wa mipaka zinazochukuliwa na mataifa mengine.