OPEC+ yakubaliana kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa kiasi kidogo

Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani, zimekubaliana kupunguza uzalishaji kwa kiwango kidogo mwezi Oktoba ili kukabiliana na kupungua kwa bei za mafuta ghafi.

Wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao jana Jumatatu, OPEC na washirika wake waliamua kupunguza mapipa 100,000 kwa siku.

Kundi hilo ambalo Urusi ni mwanachama linajulikana kama OPEC Plus. Uamuzi wa kundi hilo kurejelea viwango vya uzalishaji vya mwezi Agosti unakuja huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kwamba uchumi wa dunia utasuasua kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha riba barani Ulaya na Marekani.

OPEC Plus inabadili mwelekeo wake kutoka mkutano uliotangulia. Tangu msimu wa joto mwaka jana, kundi hilo lilikuwa likiongeza uzalishaji taratibu ili kukidhi mahitaji yaliyoongezeka baada ya janga la virusi vya korona.

Wachambuzi wanasema nchi zinazozalisha mafuta zinahadhari juu ya hatua inayopigwa kwenye majadiliano ya nyuklia kati ya nchi zenye nguvu duniani na Iran. Hii ni kwa sababu makubaliano ya nyuklia na Iran huenda yakasababisha kuongezeka kwa kiwango cha mafuta yanayosambazwa na nchi hiyo.