Kimbunga Hinnamnor chaelekea kaskazini juu ya bahari nje ya eneo la Chugoku nchini Japani

Kimbunga kikubwa na kikali cha Hinnamnor kinaelekea upande wa kaskazini juu ya bahari nje ya eneo la Chugoku magharibi mwa Japani.

Maafisa wa utabiri wa hali ya hewa nchini humo wanasema kufikia leo Jumanne mchana, kimbunga hicho kilikuwa kikielekea kaskazini mashariki juu ya bahari kilomita 280 nje ya kaskazini-kaskazini magharibi ya mji wa Matsue mkoani Shimane kwa kasi ya kilomita 60 kwa saa.

Kimbunga hicho kilisababisha mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya Japani.

Hali ya angahewa inatarajiwa kusalia kutokuwa thabiti hadi mwishoni mwa leo Jumanne magharibi mwa Japani na hadi kesho Jumatano mashariki mwa nchi hiyo. Maafisa wa hali ya hewa wanatoa wito wa tahadhari dhidi ya mvua ya radi na mvua kubwa itakayonyesha katika eneo hilo.

Maafisa hao pia wanatoa tahadhari kwa watu dhidi ya pepo kali, mawimbi makubwa, ngurumo, maporomoko ya ardhi, mafuriko na mito kufurika.