Maombi ya bajeti ya Japani ya mwaka wa fedha wa 2023 yakaribia rekodi

Wizara ya Fedha ya Japani inasema maombi ya bajeti ya wizara na taasisi za nchi hiyo yatazidi yeni trilioni 110, au karibu dola bilioni 780 kwa mwaka wa pili mfululizo.

Wizara hiyo inasema maombi ya mwaka wa fedha wa 2023 unaoanza mwezi Aprili yalitolewa kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita. Kiwango cha jumla ni cha pili tu kutoka kiwango cha mwaka wa fedha wa 2022.

Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii inaomba bajeti kubwa zaidi ya karibu dola bilioni 240.

Wizara ya Ulinzi inaomba kiasi ambacho ni rekodi cha zaidi ya yeni trilioni 5.5 au takriban dola bilioni 40. Ombi hilo linajikita kwa mpango wa serikali wa kuimarisha haraka uwezo wa ulinzi ndani ya miaka mitano.

Viwango vya kina havikutolewa kwa baadhi ya nyanja ikiwemo ulinzi na juhudi za kuhamasisha uchumi wa kijani, hivyo kiwango cha jumla cha mwisho kinaweza kuongezeka hata zaidi.