Urusi yafuta ziara zisizohitaji viza za wakazi wa zamani Wajapani kwenye visiwa vinne

Urusi inasema imefutilia mbali makubaliano ya pande mbili na Japani yanayoruhusu wakazi wa zamani wa Japani katika visiwa vinne vinavyoshikiliwa na Urusi kuzuru visiwa hivyo bila viza.

Urusi inavidhibiti visiwa hivyo vinne. Japani inadai kuvimiliki. Serikali ya Japani inasema visiwa hivyo vilitwaliwa kinyume cha sheria baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Jana Jumatatu, serikali ya Urusi ilitoa tangazo la upande mmoja la kufutwa kwa makubaliano hayo. Ikulu ya nchi hiyo iliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuitaarifu serikali ya Japani.

Inaaminika kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kulipiza kisasi vikwazo ambavyo Urusi iliwekewa na Japani kufuatia uvamizi wa Ukraine.

Mnamo mwaka 1991, Japani na Urusi zilikubaliana juu ya kile kinachojulikana kama mpango wa mabadilishano wa visiwa vinne. Mpango huo uliruhusu ziara zisizohitaji viza ili kuhamasisha mabadilishano kati ya wakazi wa zamani na wa sasa wa visiwa hivyo.

Mnamo mwaka 1999, makubaliano ya ziada yanayoitwa ziara zisizohitaji viza yalifikiwa na kuruhusu wakazi wa zamani na jamaa zao kuzuru miji yao ya nyumbani visiwani hapo.

Takriban Wajapani na Warusi 30,000 wameshiriki mabadilishano hayo.