Zelenskyy: Vikosi vya Ukraine vimetwaa maeneo kusini na mashariki

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema vikosi vyake vimetwaa tena maeneo mawili yaliyopo kusini na moja mashariki mwa nchi hiyo.

Zelenskyy alitoa tangazo hilo kupitia ujumbe wa video uliotolewa jana Jumapili.

Alisema vikosi vya Ukraine "vilichukua hatua nzuri, vikasonga mbele na kurejesha matarajio fulani" katika eneo linaloanzia Lysychansk katika mkoa wa mashariki wa Luhansk hadi Siversk katika mkoa jirani wa Donetsk.

Urusi ilitangaza mwezi Julai kuwa imechukua udhibiti kamili wa eneo la Luhansk.

Zelenskyy pia alisema vikosi vya Ukraine vilikomboa eneo huko Donetsk na kusisitiza nia yake ya kuongeza mapigano eneo la mashariki.