Uingereza: Vikosi vya Urusi nchini Ukraine vyakosa motisha

Vikosi vya Ukraine vinaongeza mashambulizi kusini mwa nchi hiyo ili kutwaa tena eneo lililochukuliwa na Urusi. Wakati huo huo vikosi vya Urusi vinaripotiwa kukumbwa na upunguaji wa motisha na nidhamu huku mzozo ukiendelea.

Ukraine ilianza kampeni ya kijeshi ya hivi karibuni katika eneo la Kherson na maeneo mengine mwezi Agosti. Vyombo vya habari vya nchini humo jana Jumapili viliripoti kwamba vikosi vya Ukraine vilishambulia ghala la silaha la Urusi na kurejesha baadhi ya maeneo.

Mchambuzi mmoja kutoka Wizara ya Ulinzi ya Uingereza anasema vikosi vya Urusi nchini Ukraine vinaonekana kupungukiwa motisha na nidhamu.

Katika taarifa zake za mara kwa mara za kiintelijensia jana Jumapili, Wizara hiyo ya Ulinzi ilisema vikosi vya Urusi havijapatiwa silaha za kutosha na chakula kwa sababu ya uchelewaji wa usambazaji.

Kadhalika wizara hiyo iliripoti kuwa vikosi vya Urusi huenda vinakumbwa na “matatizo makubwa ya kutolipwa bonasi ya kutosha ya mapambano.”