Meli za kijeshi za Urusi na China zarusha risasi kwenye bahari ya Japani

Wizara ya Ulinzi ya Japani inasema meli sita kutoka jeshi la majini la Urusi na China zimerusha risasi kwenye bahari ya Japani. Inashuku kwamba kitendo hicho ni sehemu ya mazoezi makubwa ya kijeshi ya Urusi.

Wizara inasema Kikosi cha Kujihami cha Majini cha Japani kilithibitisha kuwa manowari tatu za Urusi na meli tatu za China zilisafiri majini kuelekea mashariki umbali wa takribani kilomita 190 magharibi ya Rasi ya Kamui kwenye mkoa wa kaskazini kabisa mwa Japani wa Hokkaido juzi Jumamosi mchana. Aidha inasema meli za China zilijumuisha manowari.

Wizara hiyo inasema meli hizo sita zilirusha risasi kwenye maji jirani na mahali zilikoonekana. Inaongeza kwamba meli hizo baadaye zilipita kwenye Mlango Bahari wa Soya na kuingia katika Bahari ya Okhotsk.

Alhamisi iliyopita Urusi ilianza mazoezi ya wiki moja ya kijeshi yaitwayo Vostok katika Bahari ya Japani na maeneo mengine. Yanajumuisha vikosi kutoka China na nchi zingine.

Wizara ya Ulinzi ya Japani inaendelea kufanya doria na kufuatilia.