Kongamano la kimataifa la uchumi linalofadhiliwa na Urusi kuanza Vladivostok

Kongamano la kimataifa la kiuchumi linalofadhiliwa na Urusi linatarajiwa kuanza katika Mashariki ya Mbali nchini humo leo Jumatatu huku kukiwa na vikwazo vikali vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Kongamano la saba la Kiuchumi la Mashariki huko Vladivostok inaripotiwa kutarajiwa kuvutia washiriki kutoka nchi na maeneo zaidi ya 60. Linajumuisha wawakilishi wa wafanyabiashara na maafisa wa serikali. Rais wa Urusi Vladimir Putin atahudhuria pia.

Mada kuu ya kongamano hilo la siku nne la mwaka huu ni "Kuelekea njia yenye nchi zenye nguvu nyingi Duniani." Maafisa wa Urusi wanatarajiwa kutumia mkutano huo kujadili jinsi ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano wa Shanghai, ambalo linaongozwa na China na Urusi na Umoja wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia.

Putin alituma ujumbe wa salamu kwa kongamano hilo wiki iliyopita akisema, "Mtindo wa zamani wa taifa moja kutawala dunia unabadilishwa na mpangilio mpya wa ulimwengu."

Ujumbe huo pia ulionyesha kwamba anatilia maanani uhusiano na nchi za eneo la Asia Pasifiki, haswa nchi ya China.