Polisi nchini Canada wawasaka washukiwa wawili kufuatia mauaji ya visu

Polisi nchini Canada wanawasaka wanaume wawili kufuatia shambulio la kuwachoma kwa visu na kuwasababishia vifo takribani watu 10 na wengine 15 kujeruhiwa katika jimbo la Saskatchewan katikati mwa nchi hiyo.

Polisi wanasema mashambulizi hayo yalitokea katika maeneo 13 jana Jumapili. Wamewataja wanaume wawili wenye umri wa miaka 30 na 31 kuwa washukiwa.

Polisi hao wanasema baadhi ya wahanga wa tukio hilo inaonekana walilengwa na washukiwa hao, lakini wengine inaonekana walishambuliwa kiholela.

Washukiwa hao wanaaminika kuwa na silaha. Polisi wametoa wito kwa wakazi kusalia majumbani na kuwataka washukiwa kujisalimisha.

Waziri Mkuu Justin Trudeau alituma ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter unaosema, "Mashambulizi huko Saskatchewan leo ni ya kutisha na ya kuhuzunisha. Ninawafikiria wale waliopoteza wapendwa wao na wale waliojeruhiwa."

Mnamo mwaka wa 2020, mtu mwenye bunduki alifyatua risasi katika mkoa wa mashariki mwa Canada wa Nova Scotia, na kuua watu wasiopungua 19.