Kimbunga Hinnamnor chakaribia Kyushu kaskazini

Kimbunga kikubwa na chenye nguvu cha Hinnamnor kinahofiwa kuleta pepo kali na mvua kubwa hasa eneo la kaskazini mwa Kyushu na mkoa wa Yamaguchi uliopo magharibi mwa Japani.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Japani inasema kwamba kufikia saa saba mchana leo Jumatatu kwa saa za nchini humo, kimbunga hicho kilitarajiwa kuelekea kaskazini juu ya Bahari ya China Mashariki kwa kasi ya karibu kilomita 20 kwa saa.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea kaskazini mashariki juu ya bahari hiyo na kukaribia kaskazini mwa Kyushu kuanzia leo Jumatatu jioni hadi kesho Jumanne asubuhi.

Hadi kufikia kesho Jumanne, kaskazini mwa Kyushu huenda kukawa na pepo kali zenye kasi ya hadi kilomita 144 kwa saa na dhoruba yenye kasi ya kilomita 216.

Maafisa wa hali ya hewa wanatoa tahadhari dhidi ya dhoruba na mawimbi makubwa pamoja na maporomoko ya ardhi, mafuriko katika maeneo ya mabondeni na mito kufurika.