Wajerumani waingia wasiwasi juu ya kusitishwa kwa usambazaji wa gesi ya Urusi

Watu nchini Ujerumani wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusiana na usitishaji zaidi wa usambazaji wa gesi asili kutoka Urusi baada ya kampuni kubwa ya nishati ya Urusi Gazprom kutangaza bomba kubwa la gesi kuelekea Ujerumani litaendelea kusitishwa.

Gazprom ilisitisha usambazaji wa gesi kwenye bomba la Nord Stream mwishoni mwa mwezi Agosti kwa kile ilichosema siku tatu za matengenezo.

Kwa sasa kampuni hiyo inasema haitarejesha usambazaji wa gesi kama ilivyopanga, ikigusia kuvuja kwa mafuta kulikobainka juzi Ijumaa.

Maelezo hayo yalitiliwa mashaka na kampuni ya Ujerumani ya Siemens Energy, ambayo ilishiriki katika matengenezo. Siemens inasema uvujaji haujumuishi sababu za kiufundi za kuzuia gesi kupita.

Watu nchini Ujerumani wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusiana na muda mrefu wa kusitishwa kupatiwa gesi.

Jijini Berlin, baadhi ya raia wanasema Urusi inatishia kuharibu maisha yao. Wengine wanasema watajaribu kuhifadhi gesi wakati bei zikitarajiwa kuongezeka zaidi.

Kampuni ya Gazprom imepunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wa gesi kupitia bomba. Mataifa ya Ulaya ambayo yanategemea gesi ya Urusi yanasema nchi hiyo inatumia nishati hiyo kama silaha ya kujibu vitendo vyao ikiwa ni mwitikio wa uvamizi wa Ukraine.

Mataifa ya Ulaya yanatoa wito kwa raia kuhifadhi nishati. Lakini wasiwasi unazidi kuongezeka juu ya iwapo kutakuwa na mafuta ya kutosha wakati msimu wa baridi kali ukikaribia na mahitaji kuongezeka.