Erdogan amwambia Putin: Uturuki inaweza kuratibu utatuzi wa mtanziko wa kituo cha nyuklia cha Ukraine

Ofisi ya rais wa Uturuki imesema Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo alizungumza na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwa njia ya simu na kumweleza kuwa nchi yake imenuwia kuratibu mazungumzo ya kutatua mkwamo katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia wa nchini Ukraine.

Ofisi hiyo ya rais ilitoa tamko hilo baada ya viongozi hao wakuu kuzungumza jana Jumamosi. Ilisema rais wa Uturuki alionyesha kuchukua jukumu hilo la usuluhishi, kama alivyofanya katika utatuzi wa makubaliano kuhusu nafaka ya Ukraine.

Ofisi ya rais wa Urusi ilisema viongozi hao wawili walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwenye sekta kama vile nishati na uchumi.

Pia ilisema kuwa Erdogan alitoa salam zake za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa mwisho wa Kisovieti, Mikhail Gorbachev, ambaye mazishi yake yalifanyika jana Jumamosi.