Japani yashuhudia msimu wa pili wa joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa

Maafisa wa hali ya hewa nchini Japani wamesema kuwa nchi hiyo imeshuhudia msimu wa pili wa joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya nchi hiyo imetoa taarifa hiyo kwa kuzingatia takwimu za kuanzia mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu. Imesema kuwa, wastani wa kiwango cha joto uliongezeka kwa nyuzijoto 0.91 za selsiyasi zaidi ya kiwango cha kawaida.

Kiwango hicho ni cha pili kwa ukubwa tangu nchi hiyo ilipoanza kutunza takwimu za viwango vya joto mnamo mwaka 1898. Kiwango cha juu kabisa kilirekodiwa mwaka 2010.

Viwango vya juu zaidi vya joto viliripotiwa hasa maeneo ya mashariki na magharibi mwa Japani, na pia katika maeneo ya Okinawa na Amami.

Ripoti hiyo pia inasema, wastani wa joto kwenye uso wa bahari katika maeneo ya maji ya jirani na Japani kwa msimu huu wa joto ulipanda kwa nyuzijoto 0.8 zaidi ya kiwango cha kawaida. Kiwango hicho ni cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa tangu utunzaji wa takwimu za aina hiyo ulipoanza mnamo mwaka 1982, sawa na mwaka 2001 na 2016.