Japani yaiomba Australia kuhakikisha usambazaji thabiti wa gesi kufuatia uwezekano wa kupunguza mauzo ya nje

Japani imeiomba Australia kuendelea kuisambazia gesi asilia ya kimiminika kwa namna thabiti, wakati huu ambapo Australia inafikiria kupunguza mauzo yake ya nje ya bidhaa hiyo kufuatia uwezekano wa uhaba wa usambazaji.

Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japani, Nishimura Yasutoshi, alikutana na Waziri wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Nishati wa Australia, Chris Bowen, jana Ijumaa. Wawili hao walikutana pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa nishati wa nchi wanachama wa kundi la nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G20, unaoendelea kwenye Kisiwa cha Bali, nchini Indonesia.

Australia ndiyo msambazaji mkubwa wa gesi asilia ya kimiminika kwa Japani, ambapo inatoa takribani asilimia 35 ya mauzo yake.

Nishimura alisema usalama wa nishati kwa sasa unapitia kipindi kigumu kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine. Alisema kuwa, anataka kufanya majadiliano ya wazi na Bowen, kwakuwa Australia ni mshirika muhimu zaidi wa Japani katika maliasili na nishati.

Kwa upande wake, Bowen alionyesha kuyaelewa maoni ya Japani.

Serikali ya Australia inapanga kuamua iwapo itaidhinisha mauzo ya nje ya bidhaa hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Serikali ya Japani itaendelea na majadiliano kutathmini athari zinazoweza kutokea.