G7 kuweka ukomo wa bei kwa mafuta ya Urusi

Mawaziri wa fedha kutoka Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani-G7 wamekubaliana kuweka ukomo wa bei kwa mafuta ya Urusi kuanzia mwezi Disemba mwaka huu. Hatua hiyo inalenga kupunguza uwezo wa Urusi kufadhili uvamizi wake nchini Ukraine.

Mawaziri hao walitoa tangazo hilo jana Ijumaa baada ya mkutano wao uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Walisema hatua hiyo itatekelezwa kwa mafuta ya baharini ya Urusi na bidhaa za petroli, na inalenga pia kukabiliana na ongezeko la bei za nishati duniani.

Katika taarifa yao, mawaziri hao walizisihi nchi zingine zinazotaka kuagiza mafuta na bidhaa za petroli kutoka Urusi kuzingatia ukomo huo wa bei.

Waziri wa Fedha wa Japani, Suzuki Shunichi, aliwaambia wanahabari kwamba anapanga kufanya kazi na mawaziri wenzake na mashirika husika kutekeleza hatua hiyo.