IMF yafikia makubaliano na Sri Lanka kuikopesha dola bilioni 2.9

Wajumbe waliotumwa nchini Sri Lanka na Shirika la Fedha Duniani, IMF wamefikia makubaliano ya awali ya kuipa nchi hiyo mkopo wa karibu dola bilioni 3 huku mdororo wa uchumi ukitokota nchini humo.

IMF inasema mkopo huo mpya utakaolipwa kwa kipindi cha miaka minne unalenga kuhakikisha uthabiti wa uchumi mkuu wa nchi hiyo na kumudu ulipaji wa mikopo. Deni la nje la Sri Lanka liliongezeka hadi zaidi ya dola bilioni 50 mwishoni mwa mwaka jana.

Mwezi Aprili, Sri Lanka ilitangaza kusitishwa kwa malipo ya madeni yake ya nje kufuatia mdororo mkubwa wa uchumi uliosababishwa na kupungua kwa hifadhi za ubadilishanaji wa fedha za kigeni.

Watu nchini humo wanakabiliwa na mfumko wa bei unaoongezeka na uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kikiwemo chakula, mafuta na dawa.