Serikali ya Japani yaweka utaratibu wa mazishi ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa zamani Abe Shinzo

Jana Jumatano serikali ya Japani imeweka utaratibu utakaofuatwa katika mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abe Shinzo yaliyopangwa kufanyika Septemba 27.

Tukio hilo litaanza saa nane mchana, kwenye ukumbi wa Nippon Budokan jijini Tokyo. Watu hadi 6,000 wanatarajiwa kuhudhuria, wakiwemo wakuu wa Mabaraza ya Chini na ya Juu ya Bunge la Japani, jaji mkuu wa Mahakama ya Juu na Wabunge.

Viongozi wa kigeni na wawakilishi wa serikali za maeneo ya Japani na nyanja mbalimbali pia wataalikwa. Mialiko itatumwa mapema Septemba.

Wananchi wataweza kuweka maua kwenye madhabahu nje ya ukumbi huo kati ya saa nne asubuhi na saa kumi jioni siku ya mazishi.