Wasiwasi juu ya magonjwa ambukizi nchini Pakistan kufuatia mafuriko

Pakistan inatoa tena wito wa msaada wa kimataifa huku kukiwa na ongezeko la wasiwasi juu ya uwezekano wa milipuko ya magonjwa ambukizi kufuatia mafuriko kwenye maeneo mengi.

Tangu katikati ya mwezi Juni, maeneo mbalimbali nchini Pakistan yamekabiliwa na mvua kubwa zaidi kuliko wastani wa kila mwaka.

Mamlaka za maafa nchini humo zinasema hadi kufikia sasa watu 1,191 wamethibitishwa kufariki.

Mafuriko hayo yameharibu barabara na reli. Usambazaji wa chakula na dawa umekuwa mgumu.

Waziri wa Mabadiliko ya Tabia Nchi Sherry Rehman jana Jumatano alionya juu ya uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa ambukizi kama vile malaria na kipindupindu kutokana na hali mbaya ya usafi.

Waziri huyo aliwaambia wanahabari kwamba mbu wameonekana katika maeneo yaliyoathiriwa, na akaelezea wasiwasi wake kuhusu magonjwa yanayotokana na maji machafu. Aliongeza kuwa watu wengi wanaweza kuugua.

Rehman ameita mafuriko ya sasa nchini mwake kuwa maafa ya mabadiliko ya tabia nchi. Alisema Pakistan imeathiriwa na ongezeko la joto duniani hata hivyo inawajibika kwa kiasi kidogo juu ya hilo.

Alisema nchi zinazotoa kiasi kikubwa cha hewa ya kaboni dayoksaidi zinapaswa kuwajibika.