Meli za kivita za Marekani zapita Mlango Bahari wa Taiwan

Jeshi la Wanamaji la Marekani lilisema meli zake mbili za kivita zilipita katika Mlango Bahari wa Taiwan jana Jumapili.

Kamandi ya Saba ya Kijeshi ya Majini ya Marekani ilisema meli hizo USS Antietam na USS Chancellorsville zilikuwa zikisafiri "kawaida" kupitia mlango huo.

Kamandi hiyo ilisema meli hizo zilipitia ukanda wa "nje ya bahari ya eneo la nchi yoyote," na kwamba hatua hiyo inaonyesha kujitolea kwa Marekani kwa eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki.

Mara nyingi meli zake zilipita mlango huo hapo awali, lakini hii ilikuwa operesheni ya kwanza kama hiyo tangu kuongezeka kwa mvutano na China juu ya ziara ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi eneo la Taiwan mapema mwezi huu.

Jeshi la China linasema lilikuwa likifuatilia meli za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani ambazo zilipitia Mlango Bahari wa Taiwan jana Jumapili.

Kamandi ya Eastern Theatre, ambayo inashughulikia Bahari ya China Mashariki, inasema inaendelea kuwa makini na iko tayari kukabiliana na uchokozi wowote.

Marekani inachukulia mlango huo kama eneo la maji la kimataifa ambapo chombo chochote kinaweza kusafiri kwa uhuru. Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema mwezi Juni kwamba China haikubaliani.