Wajapani waliowahi kutekwa nyara Korea Kaskazini waomba mateka wengine kuokolewa mapema

Raia wawili wa Japani waliorejea nyumbani baada ya kutekwa nyara na Korea Kaskazini miongo kadhaa iliyopita wametaka watu wengine wote waliotekwa nyara waokolewe haraka iwezekanavyo.

Soga Hitomi na Hasuike Kaoru walizungumza hayo kwenye mkutano katika mkoa wa Niigata jana Jumapili.

Soga na mama yake Miyoshi walitekwa nyara na mawakala wa Korea Kaskazini kutoka mkoa huo unaotazamana na Bahari ya Japani mwaka 1978. Soga alirejea nyumbani baada ya mkutano wa viongozi wa Japani na Korea Kaskazini mwaka 2002. Lakini mama yake bado hajulikani aliko.

Hasuike pia alitekwa nyara kutoka mkoa wa Niigata mnamo mwaka 1978 na kurudi Japani mnamo mwaka 2002.

Hasuike alikanusha madai ya Korea Kaskazini kwamba raia wanane wa Japani waliotekwa nyara walikufa na mabaki ya wengi wao yamepotea katika mafuriko. Alidai wote waliotekwa nyara warudishwe haraka iwezekanavyo.