LDP yaitaka serikali kuharakisha kazi ya kuondoa dutu za mionzi huko Fukushima

Chama kikuu tawala cha Japani cha Liberal Democratic Party, LDP kimeitaka serikali kuharakisha kazi ya kuondoa dutu za mionzi katika maeneo yaliyobainishwa kama "maeneo magumu kurejea" baada ya ajali ya nyuklia katika mtambo wa Fukushima Namba Moja mwaka 2011.

Wabunge wa chama cha LDP wamekusanya mapendekezo ya kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na majanga ya tetemeko la ardhi, tsunami na nyuklia mwaka 2011.

Wanasema serikali inapaswa kuendelea kwa ufasaha na kazi ya kusafisha "maeneo magumu kurejea," ambapo maagizo ya kuhama bado yanatekelezwa.

Baadhi ya sehemu za eneo lisiloweza kuingilika tayari zimesafishwa ili kuwawezesha wakazi wa zamani kurejea.

Lakini wabunge wa LDP wanasema maafisa wanapaswa kuanza kazi ya kusafisha katika maeneo mengine baada ya kusikia kutoka kwa wakazi wa zamani na kuamua juu ya maeneo ambayo yanahitaji kusafishwa.

Wanaitaka serikali hasa kuanza kazi hiyo katika mwaka ujao wa fedha unaoanza mwezi Aprili katika sehemu za miji ya Okuma na Futaba, ambapo kuna mtambo wa Fukushima Namba Moja.