IAEA yajiandaa kutuma timu ya wataalamu kwenye mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA linajiandaa kutuma timu ya wataalamu kwenye mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini Ukraine, ambako kuendelea kwa mashambulizi ya makombora kunazua wasiwasi wa kutokea kwa ajali mbaya.

Mtambo huo umekuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Urusi tangu mapema mwezi Machi. Ni mmoja wa mitambo mikubwa zaidi ya nyuklia barani Ulaya. Umeshambuliwa kwa makombora na Alhamisi wiki iliyopita ulipoteza kwa muda umeme unaosambazwa kutoka nje ili kudumisha mfumo wa upoozaji.

Ukraine na Urusi zinalaumiana kwa kuushambulia mtambo huo.

Rafael Grossi ni Mkurugenzi Mkuu wa IAEA. Jana Jumapili, alisema anaendelea kushauriana na pande zote ili kutuma timu ya wataalamu wa IAEA kwenye mtambo huo siku chache zijazo. Ziara hiyo ya wataalamu iliyopangwa itatathmini uharibifu wa majengo ya mtambo huo, kubaini ikiwa mifumo ya usalama inafanya kazi na kutathmini mazingira ya kazi ya wafanyakazi.