TICAD yaangazia umuhimu wa 'fedha thabiti za maendeleo'

Viongozi kutoka Japani na nchi za Afrika katika Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, TICAD 8, wamesisitiza umuhimu wa kile wanachokiita "fedha thabiti za maendeleo." Hii inakuja wakati China imekuwa ikitoa mikopo mikubwa kwa mataifa ya Afrika.

Viongozi hao walipitisha Azimio la Tunis na kuhitimisha mkutano huo nchini Tunisia jana Jumapili.

Azimio hilo linaita uwekezaji wa sekta binafsi kuwa ni "muhimu kwa maendeleo na ukuaji shirikishi na endelevu wa uchumi barani Afrika."

Linasema viongozi hao wanasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Japani na Afrika ili kukuza uvumbuzi kutoka sekta binafsi kupitia uhamishaji wa teknolojia na kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu viwandani.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio alizungumza kwa njia ya mtandao katika mkutano wa pamoja na wanahabari katika TICAD jana Jumapili. Alifuta safari yake ya kuhudhuria mkutano huo ana kwa ana baada ya kukutwa na maambukizi ya virusi vya korona.

Kishida alisema Japani inatamani kuwa mshirika anayekua pamoja na Afrika. Alisema Japani inachangia pakubwa katika maendeleo ya bara hilo kwa kukabiliana na changamoto kwa pamoja.