Seneta wa Marekani awasili Taiwan licha ya pingamizi za China

Seneta wa Marekani Marsha Blackburn amewasili katika eneo la Taiwan na kuifanya hiyo kuwa ziara ya tatu ya wabunge wa Marekani katika eneo hilo mwezi huu. Hii ni licha ya pingamizi za China kwa ziara kama hizo.

Ndege iliyombeba Blackburn ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican kutoka jimbo la Tennessee, ilitua katika uwanja wa ndege wa Taipei jana Alhamisi usiku.

Ofisi ya rais wa Taiwan na Wizara ya Mambo ya Nje zinasema seneta huyo atakutana na Rais Tsai Ing-wen na viongozi wengine wakati wa ziara yake ya siku tatu ili kujadili masuala kama vile usalama pamoja na uhusiano wa kiuchumi na kibiashara.