Mvua zaongeza hatari ya maporomoko ya ardhi na mafuriko nchini Japani

Maafisa wa hali ya hewa wa Japani wanaonya juu ya uwezekano wa kutokea maporomoko ya ardhi na mafuriko kufuatia hali za angahewa kusalia kukosa uthabiti katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Mawingu ya mvua yanajikusanya, hususani magharibi mwa Japani. Mji wa Kushimoto katika Mkoa wa Wakayama ulikuwa na mvua za hadi milimita 95 kati ya muda wa saa mbili hadi saa tatu asubuhi leo Alhamisi.

Jiji la Shimonoseki katika Mkoa wa Yamaguchi lilipata mvua za milimita 234 katika kipindi cha saa 12 hadi 11:30 alfajiri, rekodi ya juu tangu idara hiyo ilipoanza kuchukua data mahali hapo.

Ngurumo na mvua za maeneo zinatabiriwa kuanzia kaskazini mashariki hadi kusini magharibi mwa Japani.

Kaskazini mwa Kyushu kunaweza kutarajia mvua ya milimita 180 katika kipindi cha saa 24 hadi kesho Ijumaa asubuhi, wakati maeneo ya Kinki na Kanto-Koshin yanaweza kupata mvua ya hadi milimita 100.

Mvua kubwa imenyesha kwenye maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini kando ya Bahari ya Japani.

Maafisa wa hali ya hewa wanahimiza kuchukua tahadhari dhidi ya maporomoko ya ardhi, mafuriko kwenye maeneo ya mabondeni, mito kufurika, radi, upepo mkali na mvua ya mawe.