Viongozi wa NATO wathibitisha kuendelea kuisaidia Ukraine

Viongozi wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO wamesisitiza umoja wa muungano wao na kuthibitisha kuendelea kuisaidia Ukraine katika azimio la mkutano wao.

Azimio hilo limepitishwa jana Jumatano kwenye mkutano wa viongozi hao jijini Washington nchini Marekani.

Viongozi hao wamesisitiza umoja na mshikamano dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, wakisema “wanaunganishwa na maadili ya pamoja: uhuru wa mtu binafsi, haki za kibinadamu, demokrasia na utawala wa sheria.”

Wamekubaliana kuimarisha jukumu la NATO la kuisaidia Ukraine na kuratibu utoaji wa vifaa vya kijeshi na mafunzo kwa wanajeshi wa Ukraine.

Azimio hilo linasema viongozi hao “wanalaani kwa maneno makali sana yamkini” mashambulizi ya Urusi kwa watu wa Ukraine, ikiwemo hospitali ya watoto jijini Kyiv, yaliyofanyika Jumatatu wiki hii. Linataka Urusi iache vita mara moja.

Katika azimio hilo, viongozi hao pia wameiita China “mwezeshaji muhimu” juu ya vita vya Urusi nchini Ukraine, na kuongeza kwamba vitendo vya China vinaongeza tishio ambalo Urusi inaweka kwa jirani zake na usalama wa Yuro-Atlantiki.

Wameitaka China kuacha usaidizi wote wa nyenzo na wa kisiasa katika juhudi za vita vya Urusi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa vitu na malighafi zinazoweza kutumiwa kijeshi.