Vyombo vya habari vya Marekani: Maoni ya Pelosi yanaashiria Biden anapaswa kufikiria upya kugombea tena

Vyombo vya habari vya nchini Marekani vimeripoti kwamba Spika wa zamani wa Bunge la nchi hiyo Nancy Pelosi anaashiria kuwa Rais Joe Biden anapaswa kufikiria tena kusalia katika kinyang'anyiro cha urais.

Pelosi, mshirika wa muda mrefu wa Biden, alifanya mahojiano na MSNBC jana Jumatano, huku Biden akikabiliwa na wito unaoongezeka wa kujitoa katika kinyang’anyiro hicho baada ya kufanya vibaya katika mdahalo wa televisheni dhidi ya Rais wa zamani Donald Trump.

Alipoulizwa kama anamuunga mkono Biden, Pelosi alisema: "ni juu ya rais kuamua kama atagombea. Tunamtia moyo kufanya uamuzi huo kwa sababu muda sio rafiki.”

Nyota wa Hollywood, George Clooney, mwanachama wa muda mrefu wa chama cha Democrat ambaye ni mshiriki mwenza aliyeendesha hafla kubwa ya uchangishaji fedha kwa ajili ya Biden mwezi Juni, alitoa wito kwa rais huyo kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Clooney aliandika kuhusu hafla hiyo katika makala ya The New York Times iliyochapishwa jana Jumatano, akisema Biden alikuwa "mtu yule yule tuliyemshuhudia sote kwenye mdahalo."

Mwigizaji huyo alisema, "Hii ni kuhusu umri." Aliongeza, "Hatutashinda Novemba na rais huyu."

Biden alitoa hotuba katika mkutano wa chama cha wafanyakazi jana Jumatano. Alizungumzia bei za vyakula na pango kuwa juu sana, na akasema, "Tuna mambo mengi ambayo tutayafanya kwa msaada wenu katika muhula wa pili.”