Maswali na Majibu: Usalama wa viyoyozi na feni (2)

(2) Kushuka ubora wa vifaa baada ya muda

NHK inajibu maswali yanayohusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Nchini Japani, hatuna budi ila kutegemea viyoyozi na feni za umeme kuepuka ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali wakati wa miezi yenye joto kali wakati wa msimu wa joto. Lakini uzee na saa nyingi za kuendelea kuvitumia kunaweka mzigo kwa vifaa hivi na kusababisha ajali kwa mfano kushika moto. Katika kipengele hiki, tunaangazia hatari zinazoweza kutokana na viyoyozi na feni. Leo tutaangazia kushuka ubora wa vifaa hivi baada ya muda.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini ama NITE inasema kwamba jumla ya ajali 403 zinazohusiana na viyoyozi na feni za umeme ziliripotiwa katika kipindi cha miaka mitano hadi Machi 2024. Zaidi ya nusu ya visa hivi vilisababishwa na vifaa ambavyo vilitengenezwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Vifaa vilivyozeeka vinaweza kuwa na matatizo yanayosababishwa na kushuka ubora kwa sehemu za vifaa na vinakuwa katika hatari kubwa ya kuleta ajali.

Mwezi Septemba mwaka 2020, kompresa ya kiyoyozi ambacho kilikuwa kikitumika kwa miaka 33 ilishika moto mkoani Aichi. Sehemu ya kuzuia kupita kwa umeme inaaminika iliharibika na kusababisha hitilafu.

Mwezi Agosti mwaka 2021, feni ya umeme ambayo ilitumika kwa zaidi ya miaka 47 ilishika moto mkoani Shizuoka. Hii pia ilitokana na sehemu ya kifaa kama hiyo kuharibika ambayo ilisababisha hitilafu.

NITE inatoa wito kwa watumiaji kuangalia hali yoyote isiyo ya kawaida, hasa wanapotumia vifaa vya zamani.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 10, 2024