Modi akutana na ‘rafiki mpendwa’ Putin

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amefanya ziara jijini Moscow nchini Urusi wakati viongozi wa NATO wakikutana jijini Washington nchini Marekani kuangazia vita nchini Ukraine. Modi anamkubali Rais Vladimir Putin kama “rafiki mpendwa” huku viongozi wa NATO wakijaribu kumtenga.

Putin alizungumza na Modi jana Jumanne ili kuangazia namna ya kuongeza ushirikiano katika biashara, teknolojia na usalama. Alisema biashara kati ya nchi zao iliongezeka mwaka jana kwa zaidi ya asilimia 60, na aliuita ushirikiano huo kuwa wenye “faida kubwa ya kipekee.” Pia alimshukuru Modi kwa kudumisha mahusiano kipindi chote cha mgogoro nchini Ukraine.

Modi alimwambia Putin kuwa wanahitaji kutafuta njia ya amani mapema iwezekanavyo. Alisema yupo tayari kusaidia kwa njia yoyote. Modi alisema, “suluhisho haliwezi kupatikana kwenye uwanja wa mapambano. Huku kukiwa na mabomu, bunduki na risasi, suluhu na mazungumzo ya amani haviwezi kufanikiwa.”