Vifo vilivyosababishwa na maporomoko ya ardhi nchini Indonesia vyafikia 23

Watu wasipoungua 23 kwa sasa wamethibitishwa kufariki na wengine 33 hawajulikani walipo kwenye kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia, ambako mvua kubwa zilisababisha maporomoko ya ardhi. Waokoaji bado wanatafuta manusura.

Janga hilo lilitokea Jumapili iliyopita kwenye mgodi unaoendeshwa kinyume cha sheria katika Jimbo la Gorontalo, kaskazini mwa Sulawesi. Wengi wa walioathirika wanaaminika kuwa ni wachimbaji wa madini na wakazi.

Manusura, Rikson Buhungo, alisema watu walifunikwa ghafla na matope ya maporomo ya ardhi. Alisema kisha alipata kiwewe kiasi kwamba hakuwa na muda wa kwenda kuwaokoa wengine. Alisema aliweza tu kupiga kelele pale maporomoko ya ardhi yalivyoanza kumviringisha.

Mamlaka zinaendelea na operesheni za kutafuta na kuokoa. Lakini zinasema maporomoko ya ardhi yalifunga barabara na kukwamisha jitihada zao.

Mamlaka za nchi hiyo zinawasihi watu kusalia katika hali ya tahadhari. Zinasema mvua kubwa zinaweza kuendelea.