Urusi yakubali kuwaachilia Wahindi wanaopigania jeshi la Urusi

Urusi imekubali ombi kutoka India la kuwaondoa raia wa India walioajiriwa kama wanajeshi na jeshi la Urusi ambao sasa wanataka kuondoka. Waliripotiwa kuajiriwa kwa ahadi za uwongo za malipo makubwa kwa siku. Badala yake, walipelekwa Ukraine kwenye uwanja wa mapambano. India ilikuwa ikitafuta kuachiliwa kwao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya India inasema raia 35 hadi 50 wa India walipelekwa kwenye uwanja wa vita, na wawili wamethibitishwa kufariki. Vyombo vya habari vya India vilisema wanajeshi hao ni pamoja na vijana wasio na kazi wanaoishi katika umasikini.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Urusi Vladimir Putin walijadili suala hilo katika mkutano wao juzi Jumanne huko Urusi.

Vyombo vya habari vya India vinaripoti kuwa wanajeshi hao wataachiliwa ndani ya wiki chache zijazo ikiwa ni mapema zaidi.

Baada ya mkutano wa Modi na Putin, waziri wa mambo ya nje wa India aliweka wazi kuwa nchi yake iliitaka Urusi kutatua suala hilo.

Huku uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ukiendelea, imethibitishwa kuwa raia kutoka India, Nepal, na nchi zingine wako mstari wa mbele wa mapigano kama vikosi vya Urusi.