Waziri Mkuu wa Uingereza asisitiza ‘huduma’ katika hotuba yake ya kwanza bungeni

Keir Starmer ameahidi kufanya kazi kwa ajili ya “bunge la huduma” katika hotuba yake ya kwanza bungeni kama waziri mkuu wa Uingereza.

Bunge hilo lilikutana jana Jumanne kwa mara ya kwanza tangu Chama cha Labour kiliposhinda kwa kishindo uchaguzi mkuu wiki iliyopita.

Chama hicho kilichukua viti 412 ama takribani theluthi mbili ya viti 650 katika Bunge na kukiondoa madarakani Chama cha Conservative kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14.

Starmer alilipongeza bunge jipya kama ni bunge lenye wabunge mbalimbali kwa minajili ya asili za watu na jinsia ambalo Uingereza haijawahi kushuhudia.

Alisema, “Sote tuna jukumu la kuonyesha kuwa siasa inaweza kuwa nguvu ya manufaa,” akiongeza kuwa, “Licha ya tofauti zetu zozote za kisiasa, ni muda sasa wa kubadili ukurasa, kuungana katika jitihada za pamoja za kuinua tena taifa na kulifanya bunge hili kuwa bunge la huduma.”