Kishida aelekea Marekani kuhudhuria mkutano wa NATO

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio leo Jumatano anaelekea nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO.

Washirika wanne wa NATO katika Indo-Pasifiki, Japani, Korea Kusini, Australia na New Zealand wamepangwa kuhudhuria mkutano huo jijini Washington nchini Marekani.

Mataifa hayo manne yanatarajiwa kuthibitisha kuwa yatapanua ushirikiano na NATO katika kukabiliana na vitisho vya mashambulizi ya mtandaoni na taarifa za uongo miongoni mwa maeneo mengine.

Pia wanafikiria kufanya mikutano kwa nyakati tofauti na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy na Rais wa Marekani Joe Biden.

Kishida anapanga kuthibitisha tena kwamba Japani itaendelea kuiunga mkono Ukraine.

Anatumai pia kuwa uhusiano wenye nguvu na NATO na nchi zingine utasababisha amani na uthabiti katika eneo la Asia ya Mashariki, pamoja na Japani, kwa kutambua kwamba usalama wa Ulaya na Asia hauwezi kutenganishwa kwa kuzingatia hatua za Urusi na China.

Kishida amepangiwa kwenda nchini Ujerumani kwa mazungumzo na Kansela Olaf Scholz baada ya kuzuru Marekani.