Manusura wa bomu la atomiki waishauri serikali ya Japani kuchukua hatua kabla ya kuadhimisha miaka 80

Kundi la manusura wa bomu la atomiki na mashirika yasiyo ya kiserikali yameishauri serikali ya Japani kuchukua hatua madhubuti katika kukomesha silaha za nyuklia kabla ya mwaka ujao wa maadhimisho ya miaka 80 ya mashambulizi ya Hiroshima na Nagasaki.

Wawakilishi wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Japani kwa ajili ya Kukomesha Silaha za Nyuklia walitembelea Wizara ya Mambo ya Nje jijini Tokyo jana Jumanne. Walikabidhi barua ya ombi kwa afisa mwandamizi wa wizara anayehusika na upunguzaji wa silaha.

Barua hiyo inabainisha kuwa Japani ina jukumu kubwa la kutekeleza wakati tishio la nyuklia likiongezeka duniani kote.

Kundi hilo pia linataka serikali ya Japani kusisitiza umuhimu wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Matumizi ya Silaha za Nyuklia. Mkataba huo unapiga marufuku uendelezaji, umiliki na matumizi ya silaha za nyuklia. Ulianza kutumika mwaka 2021. Lakini mataifa matano makubwa yenye nguvu za nyuklia, na nchi ambazo ziko chini ya mwavuli wa nyuklia wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Japani, hazijajiunga na mkataba huo.