Rais mteule wa Iran athibitisha tena kuunga mkono Urusi, vikosi vinavyoipinga Israel

Rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian amethibitisha tena kuwa uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Urusi na vikosi vinavyoipinga Israel hautabadilika chini ya uongozi wake.

Mgombea huyo mwanamageuzi aliyetoa wito wa kufanywa kwa maboresho katika uhusiano wa Iran na nchi za Magharibi, alishinda duru ya pili ya urais Ijumaa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha serikali ya Iran, Pezeshkian alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin jana Jumatatu.

Pezeshkian aliripotiwa kumshukuru Putin kwa ujumbe wake wa pongezi na kusema kuwa Iran inathamini uhusiano wake wa kirafiki na Urusi na bila shaka itauimarisha.

Iran imekuwa ikizozana na nchi za Magharibi kuhusiana na uendelezaji wake wa nyuklia na masuala mengine. Imeimarisha uhusiano na Urusi ambayo pia inapinga nchi za Magharibi kuhusiana na hali nchini Ukraine, wakati wa uongozi wa Rais wa zamani Ebrahim Raisi aliyekuwa mhafidhina mwenye msimamo mkali. Raisi alifariki kwenye ajali ya helikopta mwezi Mei mwaka huu.

Televisheni ya serikali ya Iran iliripoti kuwa Pezeshkian alituma barua kwa kiongozi wa kundi la wanamgambo wa dhehebu la Shia la Hezbollah nchini Lebanon Hassan Nasrallah akimshukuru kwa ujumbe wake wa pongezi.

Pezeshkian ameelezea nia yake ya kuendelea kuunga mkono vikosi vinavyoipinga Israel.