NATO na washirika wa Indo-Pasifiki kuboresha ushirikiano katika nyanja kama vile mashambulizi ya mtandaoni

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na viongozi wa Korea Kusini, Australia na New Zealand wanatarajia kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO keshokutwa Alhamisi nchini Marekani.

Vyanzo vya habari vya serikali ya Japani vinasema viongozi hao wanatarajiwa kukubaliana kuboresha ushirikiano katika kuitikia masuala yanayohusiana na mashambulizi mtandaoni, habari ghushi na teknolojia zinazoibuka kama vile akili mnemba, AI.

Kishida anatumai kuwa ushirikiano imara na NATO utachochea amani na uthabiti kote nchini Japani kwani anaamini kwamba usalama wa bara la Ulaya hauwezi ukatenganishwa na ule wa bara la Asia kwa kuangazia hatua za Urusi na China.

Kishida ameratibiwa kusafiri kuelekea Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo na Kansela Olaf Scholz baada ya mkutano wa NATO.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kupitia mpangokazi mpya wa usalama wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mitungo ya usambazaji wa madini muhimu wakati kukiwa na ushurutishaji wa kiuchumi wa China.