Guterres ashutumu shambulizi kubwa la Urusi nchini Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN Antonio Guterres ameshutumu shambulizi kubwa la Urusi lililofanywa nchini Ukraine jana Jumatatu.

Guterres alisema hayo katika taarifa kupitia msemaji wake kuwa mashambulizi ya makombora kwenye hospitali ya watoto na kituo kingine cha afya ni ya “kushangaza sana.”

Aliongezea, “Kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia kumepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu, na mashambulizi yoyote kama hayo hayakubaliki na ni lazima yakome mara moja.”

Baraza la Usalama la UN, litafanya mkutano wa dharura leo Jumanne kuhusiana na shambulizi hilo, kupitia ombi la Ufaransa na nchi nyingine. Urusi inashikilia urais wa zamu wa baraza hilo mwezi huu.