Shambulizi la Urusi laua watu 37 nchini Ukraine

Jeshi la Urusi limetekeleza shambulizi kubwa kote nchini Ukraine na kuua watu 37. Hospitali moja ya watoto mjini Kyiv iliharibika vibaya kufuatia shambulizi hilo.

Maeneo yakiwemo mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ya Dnipropetrovsk na Donetsk yalishambuliwa vikali jana Jumatatu.

Mjini Kyiv, majengo ya fleti na mengine yalishambuliwa kwa makombora katika maeneo saba ya mji huo. Maafisa wanasema watu 22 mjini humo waliuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.

Hospitali ya watoto ya Okhmatdyt pia ilishambuliwa. Idara ya Dharura ya Taifa nchini Ukraine ilisema shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu wawili na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.

Mamlaka za usalama nchini Ukraine ziliishutumu Urusi kwa kushambulia hospitali kwa kombora linaloongozwa.

Daktari mmoja aliyekuwa hospitalini hapo wakati wa shambulizi hilo aliiambia NHK kwamba alisikia mlipuko mkubwa na vioo vilivyovunjika vya dirisha nusra vimwangukie. Alisema daktari mwenzake alifariki na kwamba shambulizi hilo lilikuwa kitendo kikubwa cha uhalifu.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii jana Jumatatu kuwa vikosi vya Urusi vilishambulia viwanda vya kijeshi vya Ukraine na kambi za anga kwa kutumia silaha za masafa marefu zinazolenga maeneo kwa usahihi. Wizara hiyo iliongeza kuwa huu ulikuwa mwitikio wa majaribio ya Ukraine ya kushambulia vituo vya nishati ndani ya Urusi.

Kikosi cha anga cha Ukraine kilisema kilidungua 30 kati ya makombora 38 ya Urusi yaliyorushwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy aliandika katika mitandao ya kijamii kuwa “dunia nzima lazima itumie dhamira yake yote hatimaye kusitisha mashambulizi ya Urusi.”