Maswali na Majibu: Tahadhari za Kupanda Mlima Fuji (8)

(8) Matatizo ya kiafya

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji ambao ni mrefu zaidi nchini Japani, unavutia wapandaji mlima wengi raia wa kigeni kila mwaka. Lakini msongamano wa watu kupita kiasi na tabia za kutojali za wapandaji wengi zinasababisha matatizo mbalimbali, hivyo mamlaka zimetambulisha sheria mpya na hatua zingine. Katika kipengele hiki cha leo tutaangazia matatizo ya kiafya yanayohitaji tahadhari mahususi.

Unapaswa kuelewa vilivyo kwamba Mlima Fuji si rahisi kuupanda. Watu wengi wanalazimika kukatisha upandaji kutokana na ugonjwa. Kabla hujapanda unashauriwa kuwa na uelewa wa kutosha juu ya changamoto za kiafya zinazoweza kutokea.

Ugonjwa unaowapata wapandaji wengi wa Mlima Fuji mara nyingi huwa ni ugonjwa unaotokana na mwinuko unaosababishwa na kupungua kwa kiwango cha oksijeni katika damu. Wanaopatwa na ugonjwa huo huwa na dalili kama maumivu ya kichwa, kizunguzungu na kutapika. Ikiwa mgonjwa ataendelea kupanda, dalili hizo zitazidi kuwa mbaya. Tovuti rasmi ya upandaji wa Mlima Fuji inawashauri wapandaji kupumzika kwa muda mrefu kwa saa moja au mbili kwenye karibu kituo cha tano ili kuuzoesha mwili na hali ya hewa ya mwinuko. Tovuti hiyo pia inashauri kutembea kwa kasi ndogo, kunywa maji na kupumzika mara kwa mara.

Kushuka kwa joto la mwili ni ugonjwa mwingine wa kawaida. Dalili zake ni kutetemeka mwili mzima, kuhisi homa ya baridi na usingizi. Hali ikizidi kuwa mbaya mtu anapoteza fahamu na katika hali nyingine moyo na mapafu yanaweza kushindwa kufanya kazi. Ili kuepuka ugonjwa huo unashauriwa kuvaa nguo nzito za msimu wa baridi na kula vyakula vyenye kalori nyingi kama chokoleti pamoja na kunywa vinjwaji vya moto mara kwa mara.

Ukishindwa kutembea mwenyewe, tafadhali usisite kuomba msaada mapema iwezekanavyo. Unaweza kupiga simu polisi kwa namba 110 na kwa waokoaji namba 119. Pia unaweza kuwasiliana na wahudumu wa mahema ya mlimani wakuombee msaada.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 8, 2024.