Malipo yaongezeka nchini Japani, lakini uwezo wa kufanya manunuzi wapungua kwa mwezi wa 26

Wafanyakazi nchini Japani walishuhudia vipato vyao vya fedha vikipanda tena mwezi Mei, lakini uwezo wa kufanya manunuzi ulishuka kwa mwezi wa 26 mfululizo huku ongezeko la bei za bidhaa likiendelea kuzidi ongezeko la kawaida la mishahara.

Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii inasema mishahara iliyorekebishwa kutokana na mfumuko wa bei ilikuwa chini kwa asilimia 1.4 kutoka mwaka mmoja uliotangulia. Hiyo iliashiria kipindi kirefu zaidi cha kupungua tangu ulinganishaji wa data ulipoanza mnamo mwaka 1991.

Takwimu hizo zimetokana na tafiti za kila mwezi za kampuni zaidi ya 30,000 zenye wafanyakazi wasiopungua watano.

Jumla ya malipo ya wastani, ikijumuisha muda wa ziada, yamepanda kwa asilimia 1.9 mwaka baada ya mwaka hadi kufikia yeni 297,151, au dola 1,848. Hii inafikisha mwezi wa 29 mfululizo wa ongezeko.

Wizara hiyo ilisema mazungumzo ya mishahara wakati wa msimu huu wa chipukizi yalisababisha kampuni nyingi kuongeza mishahara. Hata hivyo, ilisema kupanda kwa bei za bidhaa bado ni changamoto kwa uwezo wa kufanya manunuzi.

Wizara hiyo ilisema itafuatilia kwa karibu mwenendo huo ili kuona ni lini uwezo huo unaweza kuwa imara tena, ikiongeza kuwa kampuni zingine huenda zitatoa nyongeza ya mishahara baada ya Juni.