Zelenskyy atumai viongozi wa NATO watakubali kuisaidia zaidi Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameelezea matumaini kwamba viongozi wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO watakubali kuongeza usaidizi kwa nchi yake wakati vikosi vya Urusi vikizidisha mashambulizi mashariki mwa Ukraine.

Mkutano wa viongozi wa NATO utaanza kesho Jumanne jijini Washington nchini Marekani.

Katika mtandao wa kijamii juzi Jumamosi, Zelenskyy alisema “Ili kulinda miji na vijiji vyetu vyote, na kulishinda kwa dhati tishio la Urusi, tunahitaji maamuzi madhubuti zaidi. Wiki ijayo, tutafanyia kazi uamuzi kama huo na washirika wetu.”

Nadhari inaangaziwa katika kiasi ambacho viongozi wa NATO wataweza kusaidia huku Zelenskyy akisisitiza haja ya usaidizi katika kupata makombora ya masafa marefu na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa anga.