Hali ya hewa ya joto kali yaendelea katika mikoa mingi nchini Japani

Maafisa wa hali ya hewa wa Japani wanawataka watu kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali wakati hali ya hewa ya joto kali ikiendelea kote nchini Japani leo Jumatatu. Siku zenye halijoto kali zimegharimu maisha ya watu kadhaa.

Mamalaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini humo inasema kuwa jana Jumapili joto lilipanda hadi nyuzi 40 za Selisiasi katika mji wa Shizuoka katikati mwa Japani. Ilikuwa ni mara ya kwanza halijoto kufikia kiwango hicho nchini Japani mwaka huu.

Mamlaka hiyo inatarajia halijoto kufikia nyuzi 40 za Selisiasi katika maeneo mengi ya magharibi na mashariki mwa Japani.

Mamlaka hiyo na Wizara ya Mazingira zimetoa tahadhari ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali kwa mikoa 24, ikiwa ni pamoja na Tokyo, kutoka eneo la Kanto hadi Okinawa. Maafisa wanasema viwango vya halijoto za juu na unyevunyevu vitaongeza kwa kasi hatari ya ugonjwa huo.

Watu wanahimizwa kutumia viyoyozi ipasavyo na kunywa vimiminika kama maji hata kama hawahisi kiu.

Familia zinashauriwa kutoa vipaumbele maalumu kwa wazee na watoto ambao wapo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.

Ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali huenda ndio ulisababisha vifo vya wazee kadhaa waliokuwa wakilima wakati wa joto kali.