Muungano wa mrengo wa kushoto wapata nguvu kubwa katika baraza la chini la Bunge nchini Ufaransa

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa inasema chama cha mrengo wa kushoto cha New Popular Front kimeibuka kama nguvu kubwa zaidi katika Baraza la Chini la Bunge kutokana na matokeo ya uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika jana Jumapili. Hata hivyo, hakijafikisha zaidi ya nusu ya viti.

Wizara hiyo inasema New Popular Front imepata viti 180 kati ya 577 katika Bunge la Taifa. Wizara hiyo imeongeza kuwa chama tawala cha mrengo wa kati cha Rais Emmanuel Macron kimepata viti 158, huku chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally na washirika wake kikipata viti 143.

Chama cha National Rally kilipata viti vingi katika duru ya kwanza ya uchaguzi Juni 30. Lakini chama cha New Popular Front kiliunganisha nguvu na chama tawala cha Macron kuwaunganisha wagombea kama sehemu ya jitahada zao za kupambana na National Rally katika duru ya pili.

Macron aliitisha uchaguzi wa mapema baada ya muungano wake kushindwa mno dhidi ya National Rally katika chaguzi za Bunge la Ulaya mwezi Juni.