Vifo vyaendelea kuongezeka Gaza miezi 9 baada ya kuanza kwa mapigano

Vifo vinaendelea kuongezeka katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni miezi tisa tangu mapigano makubwa yaanze kati ya vikosi vya Jeshi la Israel na kundi la Kiislamu la Hamas.

Juzi Jumamosi, jeshi la Israel lilitangaza kuwa lilifanya shambulizi la anga katika shule inayoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA huko Nuseirat katikati mwa Gaza.

Jeshi la Israel lilidai kuwa wapiganaji wa Hamas walikuwa wamejificha katika eneo la shule hiyo na kwamba ilichukua tahadhari za kupunguza hatari ya kuwadhuru raia wakati inafanya shambulio hilo.

Hata hivyo, maafisa wa afya huko Gaza wamesema watu 16 wameuawa katika shambulio hilo na wengine 50 kujeruhiwa walipokuwa wamejihifadhi kwa muda shuleni hapo.

Maafisa hao wanasema watu 38,153 wameuawa tangu mapigano hayo yaanze Oktoba 7 mwaka jana.

Mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka yanaendelea yakiongozwa na Qatar na wapatanishi wengine.