Chama cha mrengo mkali wa kulia cha Ufaransa chaelekea kupata kura nyingi katika duru ya pili ya uchaguzi

Chama cha Ufaransa cha National Rally chenye mrengo mkali wa kulia na washirika wake wanatabiriwa kupata uungwaji mkono mkubwa katika duru ya pili ya upigaji kura katika uchaguzi wa bunge nchini humo leo Jumapili.

Muungano wa National Rally ulipata zaidi ya asilimia 30 ya kura katika awamu ya kwanza ya upigaji kura katika baraza la chini la Bunge la Taifa juma lililopita.

Muungano wa mrengo wa kushoto, New Popular Front, ulishika nafasi ya pili. Muungano wa kati wa chama tawala, unaoongozwa na Rais Emmanuel Macron, ulishika nafasi ya tatu. Uchaguzi wa mapema uliitishwa na Macron mwezi uliopita.

Chaguzi za marudio zimepangwa kufanyika katika wilaya za uchaguzi za 501 kati za 577 ambako hakukuwa na mshindi katika duru ya kwanza.

Muungano wa chama tawala na New Popular Front unafanya kazi pamoja dhidi ya muungano wa vyama vyenye mrengo mkali wa kulia. Wanaunga mkono wagombea wa pamoja waliopendekezwa.

Juzi Ijumaa, taasisi ya utafiti ya Ipsos ilitoa utabiri wake uliotokana na kura ya maoni.

Ilisema muungano wa National Rally utaweza kushinda viti kati ya 175 na 205.

Inaamini kuwa New Popular Front itapata viti 145 hadi 175, na inakadiri kwamba kambi ya vyama tawala itapata kati ya viti 118 na 148.

Chama chenye mrengo wa kushoto cha New Popular Front na kundi linalopendelea mrengo wa kati vinatarajiwa kushinda viti vingi zaidi ya walivyotarajia kushinda juma lililopita, lakini huenda wakazidiwa na muungano wa mrengo mkali wa kulia.