Japani, Cambodia zakubaliana kushirikiana katika uondoaji wa mabomu yaliyotegwa ardhini nchini Ukraine

Japani na Cambodia zimekubaliana kufanya kazi pamoja kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini nchini Ukraine na nchi zingine.

Makubaliano hayo yamekuja pale Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikawa Yoko alipokutana na Naibu Waziri Mkuu wa Cambodia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Sok Chenda Sophea, katika ziara yake kwenye taifa hilo la kusini mashariki mwa Asia jana Jumamosi.

Mawaziri hao walitangaza mpango huo wa ushirikiano wa pande mbili katika uondoaji wa mabomu ardhini katika nchi zingine, ikiwemo Ukraine, kwa kuzingatia uzoefu wa miaka mingi wa Japani katika uondoaji wa silaha za kulipuka nchini Cambodia.

Hatua mahsusi ikiwemo kuanzishwa kwa timu ya kimataifa kwa ajili ya hatua za kupambana na mabomu ya ardhini nchini Cambodia.

Utengenezaji wa vifaa vya uondoaji mabomu yaliyotegwa ardhini kutafanywa kwa ushirikiano na kampuni binafsi kwa kutumia akili mnemba yaani AI na teknolojia zingine za hali ya juu.

Katika mkutano wa pamoja na wanahabari, Kamikawa alisema kwamba mabomu yaliyotegwa ardhini bado yanawataabisha watu kote duniani.

Alisema kuwa Japani imesaidia jitihada za Cambodia kuondokana na mabomu ya ardhini kwa miaka mingi. Alisema kwamba nchi hizo mbili zinaweza kufanya kazi kwa kuzingatia mbinu na maarifa zilizojikusanyia katika jitihada hizo.

Mawaziri hao wawili pia walikubaliana kushirikiana kujenga mifumo ya maji na maji taka na miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo mitandao ya 5G, pamoja na sekta za usalama wa mtandao nchini Cambodia.

Japani inapanga kuchangia kwenye maendeleo ya bandari ya Cambodia kama msingi wa usafirishaji kwenye eneo hilo.