Biden aapa kusalia katika kinyang'anyiro cha urais

Rais wa Marekani Joe Biden alisafiri hadi katika uwanja wa vita wa jimbo la Wisconsin jana Ijumaa kuwaambia wapiga kura kwamba anasalia katika kinyang'anyiro cha urais. Alitoa hotuba na kuahidi "kumshinda Donald Trump."

Biden amekuwa akiwajibu watu wanaosema ajiondoe kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu. Amesikia wito huo hata kutoka kwa wanachama wa Chama chake cha Democratic baada ya kufanya vibaya kwenye mdahalo wa televisheni wiki iliyopita dhidi ya rais wa zamani Donald Trump.

Biden alifanya mkutano jana Ijumaa katika jimbo la Wisconsin, ambapo anajaribu kushikilia kuungwa mkono na wapiga kura. Alishinda jimbo hilo katika uchaguzi wa 2020, miaka minne baada ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton kushindwa na Trump. Aliwaambia wafuasi wake "anagombea na atashinda tena."

Biden alisema hataruhusu mjadala mmoja kufuta "kazi ya miaka mitatu na nusu" na alisisitiza hatari ya kumrejesha Trump mamlakani, akimwita "tishio kubwa" kwa demokrasia katika historia ya Marekani.

Kura nyingi sasa zinaonyesha mpinzani wake akisonga mbele. Kundi linaloitwa RealClearPolitics lilitafuta wastani wa kura hizo jana Ijumaa, na kupata uungwaji mkono kwa Trump kuwa asilimia 47.5 na Biden kwa asilimia 44.2.