Joto kali kuendelea kwenye maeneo mengi ya Japani

Joto kali linatarajiwa kuendelea kwenye sehemu kubwa ya Japani leo Jumamosi. Halijoto ya hadi nyuzijoto 35 za Selisiyasi ama zaidi linatarajiwa kwenye maeneo mengi, huku joto likitarajiwa kufikia nyuzijoto 38 kwenye Jiji la Shizuoka, katikati mwa Japani.

Mamlaka ya Hali ya Hewa inasema mfumo wa mgandamizo mkubwa wa hewa kwenye Bahari ya Pasifiki utaendelea kufunika maeneo ya magharibi na mashariki mwa Japani na kusababisha joto kupanda.

Kiwango cha juu cha joto wakati wa mchana kinatarajiwa kufikia nyuzi joto 37 mjini Nakatsu katika Mkoa wa Oita.

Kiwango cha juu cha joto cha nyuzii 36 kinatarajiwa katika majiji ya Saitama, Kofu, Yamaguchi, Oita, Miyazaki na Kagoshima.

Nyuzi joto 35 zinatarajiwa kwenye jiji la Ichinoseki katika Mkoa wa Iwate, jiji la Maebashi katikati mwa Tokyo, pamoja na majiji ya Osaka, Okayama, Hiroshima, Matsuyama na Fukuoka.

Watu wanashauriwa kujizuia kufanya mazoezi makali na kutoka nje bila ya sababu za msingi, na kutumia kwa ufasaha viyoyozi.