Maswali na Majibu: Tahadhari za kupanda Mlima Fuji (7)

(7) Vifaa muhimu

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji ambao ni mrefu zaidi nchini Japani, unavutia wapandaji mlima wengi raia wa kigeni kila mwaka. Lakini msongamano wa watu kupita kiasi na tabia za kutojali za wapandaji wengi zinasababisha matatizo mbalimbali, hivyo mamlaka zimetambulisha sheria mpya na hatua zingine. Katika kipengele hiki, tunaangazia vifaa muhimu vinavyohitajika ili kupanda mlima huo.

Kwa sababu Mlima Fuji una urefu wa hadi zaidi ya mita 3,000, hali ya hewa huko inaweza ikabadilika wakati wowote. Wapandaji wanahitaji kuwa na ufahamu wa hatari mbalimbali zinazoweza kutokea. Tovuti rasmi ya upandaji wa Mlima Fuji inatambulisha vifaa vinavyohitajika katika lugha za Kijapani, Kiingereza, Kichina na Kikorea.

• Mavazi ya msimu wa baridi, ikiwa ni pamoja na kofia za akitiki na glavu ni muhimu, kwani halijoto kileleni mwa mlima huo zinaweza zikapungua hadi chini ya kiwango cha kuganda kabla ya macheo. Inapokuja kwa mavazi ya mvua, aina tofauti za mavazi yaliyotengenezwa kwa ajili ya upandaji yanapendekezwa.

• Mabuti ya kutembelea yanapendekezwa ili kuzuia maji kuingia ndani. Raba na kandambili hazistahili.

• Kunywa maji mara kwa mara ni muhimu ili kuzuia ugonjwa wa mwinuko. Hakuna kituo cha maji au maji yanayotiririka kwenye Mlima Fuji. Unahitaji lita zisizopungua 1-2 za maji ya kunywa. Unaweza ukaleta maji mengi zaidi kadiri ya uwezo wako na kununua mengine katika mahema kwenye mlima huo.

• Tovuti rasmi pia inawashauri wapandaji kuleta helmeti kwa ajili ya kutokea kwa mlipuko usiotarajiwa. Barakoa za kuzuia vumbi na miwani ya kuzuia vumbi pia ni muhimu ili kuzuia vumbi kwenye njia za mteremko.

• Tovuti hiyo pia inatoa wito kwa wapandaji kuhakikisha wanakuja na taa za kuvaa kichwani kwani huenda ukashuka mlima huo gizani kutokana na msongamano wa watu kwenye njia au kutegemea na hali yako ya afya.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 5, 2024.